Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maandamano haya yaliwakutanisha watu zaidi ya elfu moja katika jiji la Lisbon kwa ajili ya kulaani mauaji ya kimbari yanayoendelea katika Ukanda wa Ghaza na kutetea haki za watu wa Palestina. Kauli mbiu ya "Palestina Itashinda" ilikuwa ni sauti ya pamoja katika maandamano hayo. Mkusanyiko huu uliandaliwa na Baraza la Amani na Ushirikiano la Ureno, harakati za watetezi wa haki na amani kwa watu wa Palestina katika Mashariki ya Kati, na Jumuiya ya Vijana, kwa msaada wa zaidi ya taasisi 40.
Katika tamko lililotolewa katika maandamano hayo, ilitangazwa kuwa: “Israeli ni taifa la kihalifu, la kidhalimu, la kibaguzi na la kikatili ambalo kwa muda mrefu limekuwa likijitahidi kuzuia kuundwa kwa taifa la Palestina, kuwanyima Wapalestina haki ya kuishi katika ardhi yao, na kuwafukuza makwao, huku likiwazuia waliotimuliwa kurudi nyumbani kwao.” Hali hiyo hiyo, imesema taarifa hiyo, inatokea katika maeneo yote ya Palestina kama vile Jenin, Yerusalemu na katika miji na mashamba yote ya Wapalestina.
Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa: “Sasa, tishio hilo limefikia hatua ya kutangazwa kupitia midomo ya serikali ya Israel iliyo kichaa zaidi kuwahi kuonekana, huku ikipata sifa na pongezi kutoka kwa Marekani. Kuna hatari ya kutekelezwa rasmi hatua ya kuimega na kuunganisha Ukingo wa Magharibi ndani ya Israel, yote haya yanaendelea huku dunia ikiwa kimya kabisa.
Katika kipindi cha miezi 21 iliyopita, Israel imeishambulia Lebanon na Syria, ikaiharibu Yemen kwa mabomu, na hivi karibuni, mwezi uliopita, kwa kisingizio cha madai ya uongo kwamba Iran inajaribu kutengeneza silaha za nyuklia – jambo ambalo kila mtu anajua kuwa Israel haina ushahidi wowote kuhusu hilo – imeanzisha vita vya moja kwa moja dhidi ya Iran. Vita hivyo vingeweza kuisukuma dunia yote katika janga lisiloweza kufikirika kwa sababu ya madhara makubwa ambayo yangesababishwa na vita hiyo. Pamoja na hayo, Israel imeendelea kupata msaada wa kifedha na hata, katika baadhi ya matukio, shangwe na furaha kutoka kwa wafuasi wake wa kawaida.”
Kisha taarifa hiyo iliuliza kwa mshangao: “Inawezekanaje? Inawezekanaje serikali ya Ureno ikose kutamka bayana kulaani jinai hizi, na kukosa kuwa wazi katika kuwalaumu wahusika wa matendo haya mabaya, jambo linaloonyesha kwamba, Ureno haitaki kwa vyovyote kushiriki katika kukemea jinai hizi za kihistoria? Inawezekanaje serikali ya Ureno ishindwe kutetea kusitishwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israel? Inawezekanaje wakatae kutambua hadhi ya taifa la Palestina kwa sababu za kisiasa ambazo zinatufedhehesha sisi sote?” “Hatukubaliani kamwe kwamba duniani kuna maslahi yenye nguvu kiasi kwamba yanaweza kuyalinda mauaji haya kwa muda mrefu namna hii.”
Maoni yako